1.     MISINGI YA USHIRIKA (PRINCIPLES)

  1. Uanachama ulio wazi

    Uanachama katika chama cha ushirika ni wa wazi na hiari, kwa mtu yeyote anayetaka kujiunga bila kujali dini, rangi, kabila, jinsia, itikadi na yuko tayari kufuata masharti ya chama cha ushirika husika.

  2. Uongozi wa Kidemokrasia

    Chama cha ushirika huongozwa kwa msingi ya demokrasia. Wanachama hushiriki katika kutoa maamuzi ya shughuli za uendeshaji na usimamizi wa chama cha ushirika. Mfano uchaguzi wa viongozi wa Chama ikiwemo wajumbe wa bodi, kamati ya usimamizi, kupitishia makisio ya mapato na Matumizi na ama kuteua mkaguzi wa nje ni wa kidemokrasia. Hivyo wakati wa kupiga kura; ni kura moja mtu mmoja bila kujali idadi ya hisa zake chamani.

  3. Kushiriki kwa wanachama kiuchumi

    Wanachama huchangia kwa usawa katika rasilimali ya chama na kusimamia kwa misingi ya kidemokrasia matumizi ya rasilimali za chama chao. Sehemu ya rasilimali huhesabika kama mali ya pamoja na chama chao.

  4. Chama cha Ushirika ni chombo huru

    Chama cha ushirika kinaongozwa na kusimamiwa na wanachama wenyewe. Wakati wote misingi ya demokrasia inazingatiwa katika kutoa maamuzi mbalimbali na kuhakikisha uhuru wa chama unalindwa.

  5. Kutoa mafunzo, elimu na habari

    Chama cha ushirika kinatakiwa kutoa elimu na mafunzo kwa wanachama, viongozi, na watumishi ili waweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya chama chao. Chama cha ushirika kinatakiwa kitoe habari kuhusu kuwepo, na manufaa ya ushirika kwa jamii hususani vijana na viongozi (wa serikali, dini, kimila, vyama vya siasa n.k.).

  6. Ushirikiano baina ya Vyama vya Ushirika

    Vyama vya Ushirika vinahudumia Wanachama wake kwa ufanisi zaidi pale vinapoimarisha mshikamano wa wanaushirika. Hili linawezekana kwa vyama mbalimbali kuungana na kufanya kazi pamoja kuanzia ngazi ya msingi, vyama kilele, shirikisho na mpaka kimataifa. Ni wajibu wa asasi za kiushirika kujitathmini mara kwa mara kubaini shughuli ambazo zikifanyika kwa pamoja zinapunguza gharama na hivyo kumpunguzia mwanachama mzigo wa uendeshaji. Kwa mfano, shughuli za ushawishi na utetezi zinahitaji ushirikiano baina ya vyama ili ziweze kufanikiwa na kuleta tija inayokusudiwa

  7. Ushirika kujali jamii

    Vyama vya Ushirika huchangia na kuchochea maendeleo endelevu ya jamii kulingana na sera zilizokubaliwa na Wanachama wenyewe. Utekelezaji wa msingi huu unategemea hali ya makubaliano kati ya mahitaji ya jamii na matakwa ya Wanachama wa Ushirika. Haitakuwa vyema kutumia rasilimali za Wanachama kwa manufaa ya watu wasio Wanachama bila ridhaa yao. Kwa mfano, kushiriki kwenye maonyesho mbalimbali ambapo jamii inapata kujifunza namna ambavyo Chama cha Ushirika kinatakiwa kijiendeshe.